Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha,
limewapiga marufuku wanawake wajawazito kuvaa shela wakati wa kufunga
ndoa kwa madai vazi hilo ni alama ya ubikira kwa mwanamke na sio
vinginevyo.
Hayo yamesemwa na Paroko Msaidizi wa
Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresa, Padre Festus Mangwangi wakati akiweka
mkazo juu ya tamko lililotolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo Isaack
Amani, wakati akiadhimisha misa ya shukrani iliyofanyika Jumapili
iliyopita, baada ya kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francis kuwa
Askofu Mkuu wa Jimbo hilo.
Kabla ya uteuzi huo uliotangazwa Desemba
27 mwaka 2017, Askofu Mkuu Amani alikuwa Askofu wa Jimbo la Moshi na
kusema haitakiwi kwa mwanamke yeyote ambaye anajijua ni mjamzito kuvaa
shela kipindi anafunga ndoa kwa kuwa vazi hilo linavaliwa na mwanamke
asiyemjua mwanaume (bikra).
Aidha, Padre Festus Mangwangi amewataka
wazazi kuwafundisha watoto wao wa kike kutunza miili yao na kuishi
maisha ya kimaadili hadi watakapopata wenza wa kufunga nao ndoa na hapo
ndipo alama ya shela itakapoonekana umuhimu wake.
"Tamko la Askofu Mkuu linatekelezwa kwa
kuwaeleza maharusi watarajiwa wanapokwenda kupata mafundisho ya ndoa kwa
katekista na baadaye padre, kuwa kama ni wajawazito basi wasivae shela
na hata wale wanaowajua wanaume pia wanashauriwa wasivae", amesema Padre
Festus.
Pamoja na hayo, Padre Festus ameendelea
kwa kusema "wanaojitambua kuwa si bikira, hawavai shela, lakini wako
wanaojificha na kuvaa shela, hii inakuwa sawa na kudanganya".
Kwa upande mwingine, Padre Festus
amesema endapo atatokea mtu akadanganya na kuvaa shela wakati tayari
anamjua mwanaume au kuwa mjamzito basi atakuwa anafanya utovu wa
nidhamu.
No comments:
Post a Comment