Wajumbe wa Israel na wale wa Palestina wameshambuliana kwa maneno
makali katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa ulioanyika jana kwa lengo la kuzungumzia utatuzi wa vurugu na
mauaji katika ukanda wa Gaza, zinazotokana na uamuzi wa Marekani
kuhalalisha Jerusalem kuwa makao makuu ya Israel.
Zaidi ya watu 58 wameripotiwa kufa kwa kufyatuliwa risasi na askari
wa jeshi la Israel ambao wamepambana na waandamanaji wanaopinga uamuzi
huo wa Israel na mshirika wake mkuu, Marekani.
Katika mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wajumbe
kutoka Palestina walitumia maneno makali kueleza kuwa kinachofanywa na
Israel dhidi ya Wapalestina ni uhalifu dhidi ya binadamu.
Pia, walilaani vikali kitendo cha Israel inayodhibiti Jerusalem kwa
kutozingatia maamuzi ya Umoja wa Mataifa pamoja na kutozingatia
makubaliano na sheria za kimataifa.
Hata hivyo, wajumbe wa Israel walirusha lawama zote kwa kundi la
Hamas ambalo pia linadhibiti sehemu ya eneo la Gaza kwa kuwachukua
mateka Waisrael na kwamba wamekuwa wakihamasisha vurugu zilizopelekea
vifo hivyo.
Hii ni wiki ya sita ya maandamano makubwa yaliyozua ghasia,
wapalestina wakipinga uamuzi wa Israel. Watu 58 walioripotiwa kupoteza
maisha walizikwa kwa pamoja jana.
No comments:
Post a Comment