
Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa amemwambia Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila
Mkumbo kuwa anashindwa kutafuta namna ya kuwatua wamama ndoo
kichwani amekazana kuandika barua za kuwajibu maaskofu.
Msigwa amesema hayo bungeni na kudai kuwa serikali imekuwa ikipandisha
watu vyeo na kuwapa nafasi watu wengine ambao hawaendi kuleta tija
katika nafasi hizo kutokana na kukosa uzoefu wa kazi au kukosa uelewa wa
mambo, jambo ambalo amedai limepelekea halmashauri nyingi kufanya
vibaya.
"Kwenye taifa letu kunapofanyika promotion au appointment au replacement
kwenye eneo lolote haitegemeani na merits, unapomchagua Katibu Mkuu wa
wizara unamchagua kwa vigezo gani unataka akaongeze thamani gani,
unapomchagua Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya unawachagua kwa vigezo gani,
tulilalamika wakati serikali hii inaingia madarakani kwamba mmewatoa
wakurugenzi waliokuwa wazuri waliokuwa wanafanya kazi kwa waledi katika
ofisi zao lakini wakaletwa watu tu kwa sababu wanavaa sare za CCM na leo
tumeona jinsi ambavyo halmshauri zetu zinavyoshindwa kufanya kazi,
kumekuwa na ubaguzi wa hali ya juu sana na upendeleo kwa sababu hawa
wote walioteuliwa hawaendani na kazi walizopewa" alisema Msigwa
Mchungaji Msigwa aliendelea kutolea ufafanuzi hilo kwa kumtolea mfano
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo
"Kwa mfano ofisi ya Katibu Mkuu ni ofisi serious kabisa unamuona mtu
kama Prof. Kitila Mkumbo badala ya kushughulika na namna ya kumtua mama
ndoo kichwani yeye amekazana anaandika kuwajibu maaskofu ambao
wanashughulika na roho za watu mtaani, badala ya kukaa kwenye ofisi,
haya ndiyo tunayosema mtu hajui anaenda kuongeza thamani gani na
nimezungumza mambo ya replacement haya unamchukua mtu kama Kitila
anazungumzia mambo ya elimu unampeleka kwenye mambo ya maji anakaa
ofisini badala ya kuzungumza mambo ya kumtua mama ndoo kichwani ambalo
ni wazo zuri yeye anakazana anaandika anataka kumjibu askofu kwa sababu
ya mawazo aliyotoa kwamba hakuna demokrasia nchi hii" alisisitiza Msigwa
No comments:
Post a Comment