Wabunge 47 na viongozi wa dini 14, wametajwa kuwa miongoni mwa wanaume waliotelekeza wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda wanawake 480 waliofika katika ofisi yake jana, kati
yao 47 wamesema wametelekezwa na wabunge huku 14 wakieleza
wametelekezwa na viongozi wa dini.
Makonda amesema hayo leo Jumanne Aprili
10, alipokaribishwa kutoa salamu za mkoa, mbele ya Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan wakati wa hafla ya uzinduzi wa chanjo ya saratani
iliyofanyika katika viwanja vya Mbagala Zakhiem, Temeke jijini hapa.
“Wengine wamewataja wafanyabiashara mashuhuri ambao ukiwatazama huwezi kuamini kama wanafanya ukatili huu,” amesema.
Amesema takwimu zinaonesha katika mwaka
2017, walizaliwa jumla ya watoto 129,347 na kwamba asilimia 60
wametelekezwa huku katika kituo kimoja kilichopo Wilaya ya Kinondoni
pekee wanatunzwa watoto 274 ambao waliokotwa.
“Watoto hao waliokotwa wakiwa wametupwa
kwenye mifuko ya rambo kama takataka, kina mama hawa wanateseka kulipa
kodi, kununua chakula cha familia na mambo mengine.
“Kisha wengine wanasema Makonda
nahusikaje humu wakati haya ni mambo ya Ustawi wa Jamii, sisi
tunaendelea na nimeongeza siku za kuonana na kinamama hao,” amesema.
No comments:
Post a Comment