Hisia mbalimbali zimejitokeza duniani
ikiwa baadhi ya watu wanaunga mkono mashambulizi hayo na wengine kukosoa
shambulizi hilo la anga lililofanywa mapema Jumamosi na majeshi ya
Marekani, Ufaransa na Uingereza dhidi ya vituo vya serikali ya Syria.
Lakini hali ni tofauti kidogo Syria
ambapo Mamia ya wananchi wa Syria wamejitokeza katika mji mkuu wa
Damascus, Jumamosi hii wakiendesha magari huku honi zikilia,
wakionyesha alama ya ushindi na kupeperusha bendera za Syria kwa kupinga
mashambulizi ya kijeshi ya pamoja yaliyofanywa na nchi hizo tatu.
Wengine walikuwa wakipiga makelele wakisema, "Sisi ni watu wako,
Bashar."
Ndege za kivita za nchi za Ulaya na
manuari za kijeshi zilishambulia kwa makombora vituo vitatu vya silaha
za kemikali nchini Syria, shambulizi la awali ambalo linaweza kugeuka
kuwa ni muendelezo wa kampeni ya kijeshi dhidi ya serikali ya Rais
Bashar al- Assad na wanao muunga mkono.
Washirika wa Syria, ikiwemo Urusi
wamesema kuwa shambulizi hilo la pamoja dhidi ya Syria limefeli. Wizara
ya mambo ya nje imesema idadi kubwa ya makombora yaliyopigwa Syria
yaliangamizwa na mfumo ya ulinzi wa serikali ya Syria.
Katika mkutano wa waandishi wa habari
London Jumamosi, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema nia ya
kuratibu mashambulizi haya sio kwa ajili ya “kuipindua serikali,” lakini
ni “kupunguza na kuzuia” uwezo wa serikali ya Assad kutumia silaha za
kemikali.
Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa
haiwezi kusimama kando na “kutupia macho tu” wakati utawala wa Syria
ukiendelea kutumia silaha za kemikali dhidi ya watu wake.
Huko Paris, Rais wa Ufaransa Emmanuel
Macron ametoa tamko akisema, “ Hatuwezi kuvumilia kitendo cha kufanya
matumizi ya silaha za nyuklia ni mwenendo wa kawaida,” akiongeza kuwa
“ukweli wa taarifa na kuhusika kwa utawala wa Syria hauna mashaka.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
amesema anaunga mkono mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani,
Ufaransa na Uingereza.
Amesema mashambulizi hayo ya angani yaliyofanywa yanapaswa kuwa onyo kwa utawala wa Syria kutoendelea kutumia silaha za sumu.
Wakati huohuo Serikali ya Iran imesema
imesema kuwa Marekani, Ufaransa na Uingereza hazitaweza kupata manufaa
yoyote kwa kuishambulia Syria.
No comments:
Post a Comment