Maaskofu wawili wamepinga matamko yaliyotolewa hivi karibuni na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi
ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani na Makamu wa Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kibaptisti Tanzania, Michael Nhonya, wamesema viongozi
wa dini wanatakiwa kubaki kuwa walezi, washauri, wakemeaji, wenye
kuonya na kuelimisha jamii ili Watanzania waendelee kuishi kwa umoja na
amani na kuwataka wajipime wanapelekaje ujumbe wao wa kinabii kwa
viongozi wao.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi
ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani amepingana na matamko
yaliyotolewa na viongozi wa dini kuhusu mwenendo wa Serikali iliyoko
madarakani.
Akihubiri katika ibada ya Pasaka
iliyofanyika katika Kanisa la Roho Mtakatifu mjini Dodoma, Askofu
Chilongani alisema, “Hivi karibuni kumekuwa na matamko yanayotolewa na
baadhi ya viongozi wa madhehebu ... Sipo hapa kumuhukumu mtu kwa sababu
Yesu Kristu anasema msihukumu msije mkahukumiwa.”
Alisema si kusudi lake kutetea Serikali
iliyoko madarakani lakini kwa habari waliyoisoma kuna tofauti kubwa kati
ya mfalme Farao na Serikali nchini.
Askofu Chilongani alikosoa njia ya
kufikisha ujumbe kwa Serikali akisema katika Biblia, Musa alikabiliana
na Farao ana kwa ana akimtaka awaruhusu wana wa Israel waende Kanani
kumuabudu Mungu au awe tayari kupokea mapigo ya Mungu.
“Ikiwa kweli Serikali iliyopo madarakani
ina kasoro, kuna njia sahihi ya kupitia ili kuitaka ibadilike. Je, sisi
viongozi wa dini tumeshindwa kwenda Ikulu au mahali pengine popote
kukutana na viongozi wetu ambao tena ni waumini wetu hadi tukimbilie
kutoa matamko. Je, huko si kuchochea vurugu.” alihoji.
Alisema kwa miaka yote viongozi wa dini
huungana kutoa matamko ya pamoja panapokuwa na ulazima, hivyo kuhoji
inakuaje leo kila dhehebu liwe na tamko lake.
Askofu Chilongani alisema wakati huu wa Pasaka viongozi wa dini wajipime wamepelekaje ujumbe wao wa kinabii kwa viongozi wao.
Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la
Kibaptisti Tanzania, Michael Nhonya akihubiri katika ibada ya Pasaka
mjini Dodoma jana, aliwaonya viongozi wa dini kutokuwa vyanzo vya
kusababisha vurugu.
Alisema viongozi wa dini wanatakiwa
kubaki kuwa walezi, washauri, wakemeaji, wenye kuonya na kuelimisha
jamii ili Watanzania waendelee kuishi kwa umoja na amani.
Pia aliwatahadharisha Watanzania
kutojiingiza kwenye siasa zinazoashiria uchochezi unaoweza kuleta chuki
na vurugu kwa kuwa zinaweza kusababisha watu wakagawanyika.
“Viongozi wa vyama vya siasa wakae meza
mmoja kwa ajili ya maridhiano badala ya kunyoosheana vidole ambavyo
vimekuwa vikisababisha chuki miongoni mwa Watanzania,” alisema.
Alisema wakikaa pamoja wataweza kuondoa tofauti walizonazo.
Msimamo wa Askofu Shoo
Jana, akitoa salamu za Pasaka katika
Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo alisema hawataogopa kuitwa
majina yoyote na watu wanaotaka kupotosha ujumbe uliopo katika waraka
uliotolewa na maaskofu.
Alisema kuna kitu ambacho Mungu anataka
kuwaambia Watanzania kupitia waraka uliotolewa na maaskofu 27 wa kanisa
hilo pamoja na ule uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC).
Alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja
baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila
Mkumbo kumwandikia barua kiongozi huyo wa KKKT akimueleza kuwa ni muhimu
kwa kanisa kupima kwa umakini mkubwa uzito wa kila neno kabla ya kutoa
kauli kwa umma.
Profesa Kitila katika barua yake yenye
kurasa sita na maneno 2,800, alisema anatoa maoni yake binafsi akiwa ni
muumini wa kanisa hilo kuhusu maudhui ya waraka wa maaskofu hao 27 wa
kanisa hilo uliotolewa Machi 24.
Dk Shoo bila kutaja majina, alisema
baada ya waraka wa TEC na ule wa KKKT kutolewa, kuna watu wachache
wameibuka wakipotosha na kupinga, huku wengine wakidai maaskofu wanasema
kwa sababu sadaka zimepungua.
Februari 11, TEC ilitoa ujumbe wa
Kwaresima wa mwaka 2018 ndani yake maaskofu wakitoa msimamo kuhusu
masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Tangu kutolewa kwa waraka wa maaskofu wa
TEC na ule wa KKKT, kumekuwa na mijadala kadhaa nchini kuhusu
walichozungumza viongozi hao wa dini.
Dk Shoo alisema anasikitika kwamba
wanaposema jambo la ukweli linalohusu maisha ya Watanzania wote, watu
wachache wanaibuka kupotosha.
“Katika waraka tuliotoa kuna watu
wachache, nasema wajinga, wanasema maaskofu sasa wanasema kwa sababu
sadaka zimepungua kanisani, sisi sadaka hazijapungua na Wakristo
wameendelea kujitoa sana, hivyo hatujapungukiwa na kitu,” alisema Dk
Shoo.
Alisema wataendelea kusema kweli na
wanaotaka kuharibu ukweli huo waendelee kuharibu kwa kuwa Watanzania
walio wengi, wenye hekima wanaelewa maneno yaliyozungumzwa si ya
kujibiwa harakaharaka tu, bali ni ya kututafakarisha.
Alisema wataitwa majina mengi lakini
wanajua ni jitihada za upotoshaji kwa ukweli uliopo katika waraka.
Alisema si jambo la kawaida kwa maaskofu wa makanisa makubwa mawili
nchini kukaa kwa nyakati tofauti na kutoa waraka wenye ujumbe mmoja.
“Hatukukaa na kupanga tutoe waraka
lakini Baraza la Maaskofu Katoliki walikaa na kuja na waraka nasi KKKT
tukakaa tukaja na waraka ukilinganisha ujumbe ni uleule. Kuna kitu Mungu
anataka kutuambia kama Watanzania kupitia ujumbe ule,” alisema.
Dk Shoo alisema, “Mungu awaguse hao
ambao wanatumia nguvu nyingi kutaka kupotosha, wanatumia nguvu nyingi
kupaka tope ili waweze kurejea katika yale yaliyotajwa pale
wakayatafakari na kama kuna hatua za kuchukua wakachukue.”
Akitoa ujumbe wa Pasaka, Dk Shoo
aliwataka Watanzania kukataa nguvu zote zinazopinga uhuru, uhai,
kuharibu maisha ya watu na kutia hofu kwa kuwa ufufuko wa Yesu umetoa
mwanga na kuwaweka watu huru.
Alisema vitisho vya watawala vinaweza kuwafanya watoto wa Mungu wakatamani au kuendelea kukaa katika giza kutokana na hofu.
Aliwatia moyo walioelemewa na mizigo
kutokana na ukandamizaji uliopo katika mifumo mbalimbali akisema Yesu
amefufuka ili watu wote wawe huru.
Katika mahubiri yake, Askofu wa Kanisa
Anglikana Dayosisi ya Kagera, Darlington Bendankheha aliwataka watendaji
wa Serikali kutowanyamazisha viongozi wa dini, bali wakubali kukosolewa
panapoonekana kukiukwa utaratibu wa kisheria, kiimani au kiserikali.
Imeandikwa na Florah Temba (Moshi); Sharon Sauwa (Dodoma); na Shaaban Ndyamukama (Ngara) - Mwananchi
No comments:
Post a Comment