Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linatuhumiwa kuhusika na mauaji ya kijana
muuza machungwa katika soko la Sido ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Iyela II,
jijini Mbeya, anayesadikiwa kufariki katika mazingira ya kutatanisha.
Kifo cha kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Allen Mapunda (20),
kimetokea wakati ndugu wa marehemu wakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya
Kanda ya Mbeya ambapo imeelezwa kuwa kabla ya umauti marehemu alikamatwa
Machi 24, 2018 majira ya saa 4 usiku katika eneo la kucheza 'pull
table' lililopo Mtaa wa Maendeleo, na kumpeleka hadi kituo kikuu cha
Polisi ambapo alikaa kwa siku moja na kesho yake alidhaminiwa na ndugu
ambao waliamua kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu kutokana na
majeraha aliyopata.
Kwa mujibu wa mama mlezi, Alice Mapunda amesema marehemu alionekana na
majereha mkononi na kichwani ambako alikuwa akivuja damu huku
akilalamikia kupata maumivu.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga
amesema uchunguzi juu ya kifo wa kijana huyo unaendelea na kwamba
taarifa rasmi ataitoa mara baada ya uchunguzi kukamilika kwa vyombo vya
habari ili waweze kufahamu ukweli wa tukio hilo ulivyo.
No comments:
Post a Comment