Mkuu wa shule ya sekondari Kakonko
katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Peter Rubonya amefariki dunia
baada ya kujinyonga kwa kamba ofisini kwake.
Tukio hilo limetokea mapema Jumatatu Machi 26,2018 huku kukiwa na taarifa kuwa marehemu ameacha ujumbe unaosomeka "Mkurugenzi wa halmashauri ya Kakonko Lusubiro Mwakabibi asipodhibitiwa ataua wengi"
Akielezea tukio hilo , mwalimu wa zamu
Isaac Japhet amesema yeye alifika shuleni hapo mapema saa 12:30 kwa
ajili ya kuwafundisha wanafunzi wa kidato cha nne masomo ya ziada baada
ya kufunga shule wiki iliyopita, na baada ya kufika aligundua kuwa hana
chaki ambapo mkuu huyo wa shule alimpatia chaki mlinzi ili awape
wanafunzi.
Alisema baada ya muda mratibu elimu kata
pamoja na mmoja wa wazazi walifika ofisini hapo wakiwa na shida na mkuu
wa shule na baada ya kuelezwa kuwa yupo ndani ofisini waliamua kugonga
mlango ili kuingia lakini hawakuweza kujibiwa na ndipo wakaamua kufungua
mlango na kukuta mwili wa marehemu ukining’inia darini.
Mwalim Isaac amebainisha kuwa marehemu ambaye alikuwa akifundisha pia masomo ya Kemia na Fizikia
shuleni hapo hawakuwahi kusikia kuwa na mgogoro wowote wa kifamilia au
kijamii, na kwamba mkewe ambaye ni mkufunzi katika chuo kikuu cha Dodoma
UDOM alifika nyumbani kwake juzi akitokea Dodoma.
Naye mlinzi wa shule hiyo Kajoro
Kajabojabo amesema alikutana na mkuu wa shule mapema asubuhi akiingia
ofisini na kumuomba chaki ambazo alipewa na kuziwasilisha kwa walimu.
“Nilimuona kabisa tukasalimiana
nikamuuliza kama ana weza kuwa na chaki, akaingia ofisini akanipatia
boksi moja la chaki, nikachukua nikampelekea mwalimu aliyekuwa anahitaji
,alikuwa kwenye hali nzuri tu, lakini baada ya muda ndiyo tukio hilo
likatokea”aMEsema Kajoro.
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea
Ndagala akizungmza baada ya kutembelea shule hiyo na kumfariji mjane
amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kujua sababu
ikiwa marehemu aliacha ujumbe wowote au lah.
Pia ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa
jamii kutokaa na mambo yanayowasonga na badala yake wayafikishe katika
ngazi tofauti za serikali ,jamii au rafiki zao .
“Hatujajua sababu lakini ni muhimu jamii
ikajenga utamaduni wa kueleza matatizo ya ndani yanayoyasibu , hii
inasaidia sana kupunguza msongo wa mawazo na kuepusha madhara kama
haya”,amesema.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma Martin
Otieno amesema baada ya kupekuliwa kwa mwili wa marehemu huyo walikuta
karatasi imeandikwa ujumbe kuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Kakonko
Lusubiro Mwakabibi asipodhibitiwa ataua wengi.
No comments:
Post a Comment