Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
kuwapa dhamana viongozi sita wa Chadema, akiwamo mwenyekiti wake,
Freeman Mbowe, malumbano ya kisheria yanaendelea mahakamani hapo.
Washtakiwa hao wametakiwa kuwa na
wadhamini wawili ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh20 milioni na kuwa
na barua kutoka kwa viongozi wao ama wa vijiji au mtaa, ambao watapaswa
kuwa na nakala za vitambulisho vyao.
Pia, wametakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.
Hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri amesema asiyeridhika na uamuzi huo ana haki ya kukata rufaa.
Kesi hiyo inaendelea mahakamani hapo
muda huu saa tisa alasiri Machi 29, 2018 na upande wa mashtaka
unaonyesha nia ya kukata rufaa.
Mmoja wa mawakili wa viongozi wa Chadema, Peter Kibatala anaipinga taarifa ya rufaa iliyotolewa na wakili wa Serikali.
Kibatala amesema mahakama itekeleze amri
yake ya dhamana kwa kuwasainisha washtakiwa bondi ya Sh20 milioni
katika tarehe ambayo inaona inafaa, baada ya hapo ndiyo ipokee taarifa
hiyo ya Serikali ya kukata rufaa.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi
amedai kuwa hilo ni suala la kisheria kwa kuwa taarifa ya rufaa
ikishawasilishwa mahakamani na kupokelewa, mahakama husika itakuwa
imefungwa mikono kuongea chochote kuhusiana na taarifa hiyo, kwa maelezo
kuwa itakuwa imeingia katika kumbukumbu za mahakama.
No comments:
Post a Comment