Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga amesema Serikali inafanya kila liwezekanalo
kuhakikisha kuwa mmea hatari uitwao gugu karoti hauoti katika maeneo ya
hifadhi kwa kuwa una madhara makubwa kwenye malisho ya wanyamapori .
Amesema mmea huo ukiota ndani
ya maeneo ya hifadhi umekuwa ukizuia uoto asili kuota na hivyo kupelekea
kutoweka kwa malisho ya wanyamapori.
Amesema mmea huo ulibainika
miaka tisa iliyopita na umekuwaa ukisambaa katika maeneo ya nje ya
hifadhi na athari zake zimekuwa zikionekana wazi wazi.
Amesema baada ya matokeo ya
utafiti kuhusiana na mmea huo, Serikali imeamua kuiongezea bajeti
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) ili iweze kufanya tafiti
zaidi kuhusiana na mmea huo.
‘’Serikali kupitia Wizara yangu tumejipanga kuhakikisha kuwa mmea huo unatokomezwa kabisa.’’ Alisisitiza Hasunga.
Alibainisha hayo leo mjini
Arusha katika Mkutano wa utafiti wa kisayansi uliowakutanisha
Wanasayansi 300 waliofanya tafiti mbalimbali katika hifadhi za
wanyamapori na mazingira kwa ujumla wa kutoka ndani na nje ya
Tanzania.
Mkutano huo umeanza leo na
utafanyika kwa muda wa siku tatu ambapo wanasayansi watafiti mbalimbali
wataziwasilisha na kuzijadili tafiti zao zipatazo 167 katika maeneo
hayo.
Aidha, Naibu Waziri Hasunga
amesema mkutano huo utatoa nafasi ya kubadilishana uzoefu, mawazo na pia
ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii tulivyonavyo kwa wanasayansi
hao.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya
TAWIRI, Prof. Aporinalia Pereka amesema kwa upande wa Chuo cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) nao tayari wameanza kufanyia utafiti mmea huo ili
usiweze kusambaa zaidi kwa kuwa una madhara kwa wanyamapori na kwa
binadamu pia.
Amesema kwa upande wa binadamu
mmea huo umekuwa na madhara katika ngozi na upande wa wanyamapori
umekuwa ukiathiri uoto asili na hivyo kupelekea malisho ya wanyamapori
kutoweka.
Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo wa
Bodi,Prof. Pereka ameiomba serikali kupitia Wizara ya Maliasili na
Utalii iendelee kutenga bajeti ya kutosha ili Taasisi hiyo iweze
kufanya tafiti nyingi zaidi katika maeneo mengi ya nchi tofauti na sasa
inavyofanya.
No comments:
Post a Comment