Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwataarifu
wananchi kuwa inatarajia kuanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu
kwa mwaka wa masomo 2018/2019 kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi ujao
(Mei, 2018) baada ya kukamilishwa kwa maboresho makubwa ya mfumo wa
uombaji kwa njia ya mtandao.
Maboresho ya mfumo wa maombi
Mkurugenzi
Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru (pichani) amesema katika
taarifa yake leo (Jumanne, Aprili 17, 2018) kuwa maombi yote
yatapokelewa kwa njia ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz) ambao umefanyiwa maboresho na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UCC-UDSM).
Aidha,
Bw. Badru amesema dirisha hilo la litafunguliwa sambamba na kutangazwa
kwa mwongozo wa kina utakaotoa utaratibu wa kuwasilisha maombi, tarehe
ya mwisho ya kuwasilisha maombi, sifa na vigezo vitakavyotumika katika
kuchambua na kutoa mikopo kwa mwaka ujao wa masomo unaotarajiwa kuanza
mwezi Oktoba, 2018.
“Tunawasihi
wale wote wanaotarajia kuomba mkopo wa elimu ya juu kusoma kwa makini
mwongozo tutakaoutoa kwa vyombo vya habari na tovuti mwanzoni mwa mwezi
Mei, 2018 na kuuzingatia,” amesema Bw. Badru.
Bw.
Badru amefafanua kuwa wito wa Bodi ya Mikopo umetolewa kutokana na
uzoefu wa miaka iliyopita ambapo waombaji wa mikopo waliwasilisha maombi
yao bila kuzingatia mwongozo uliotolewa na kusababisha baadhi ya
wanafunzi kukosa mikopo.
“Mwaka
jana, kwa mfano, zaidi ya waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi ya
61,000 hawakuambatisha nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au hata
vile vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (RITA) kama tulivyoelekeza,” amesema.
Nyaraka muhimu zinazohitajika
Nyaraka
nyingine muhimu ambazo waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni pamoja na
nakala za vyeti vya kitaaluma za kidato cha nne, sita na stashahada
ambazo zimethibitishwa na Kamishna wa Viapo yaani Wakili au Hakimu.
Aidha,
wanafunzi waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu
wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa Mganga
Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Kituo cha Afya cha Serikali;
Bw.
Badru ameongeza kuwa wanafunzi ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya
Sekondari au Stashahada (Diploma) wawe na barua za uthibitisho wa
udhamini huo kutoka katika taasisi zilizogharamia masomo yao.
Maafisa wa HESLB kutoa elimu mikoani.
Katika
hatua nyingine, Bw. Badru amesema mwaka huu maafisa wa Bodi ya Mikopo
watatembelea mikoa mbalimbali ili kukutana na waombaji mikopo kwa lengo
la kuwaelimisha waombaji mikopo kuhusu taratibu sahihi za kuwasilisha
maombi yao ya mikopo kwa njia ya mtandao. Ratiba na maeneo itakapofanyia
mikutano hiyo itatangazwa mwanzoni mwa mwezi Mei, 2018.
HESLB
ilianza kazi rasmi mwaka 2005 ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa
mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania wahitaji na wenye sifa na
kukusanya mikopo iliyoiva ambayo ilitolewa na Serikali tangu mwaka
1994/1995.
Imetolewa na:
No comments:
Post a Comment