Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amewataka wadau wanaofanya
shughuli mbalimbali zinazohusisha na kodi ya pango kwenye Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), kuhakikisha ifikapo Februari
1, 2018 wawe wameshalipa madeni yao.
Prof. Mbarawa alisema leo wakati
alipoongea na wadau hao kwenye ukumbi wa watu Mashuhuri wa JNIA-TBII,
wakati walipozungumza nao kujadili masuala mbalimbali.
Alisema baadhi ya wadau
wameshalipa madeni yao kati ya bil 10 zilizokuwa zinadaiwa na sasa
zimesalia bil. 3.7 ambapo amewataka baada ya kumalizika kwa sherehe za
Krismas na Mwaka Mpya wahakikishe wanakamilisja madeni yao.
“Hatutasita kumuondoa mtu yeyote
atakayekuwa akiendelea kudaiwa kwani atakuwa hana sifa za kupangisha
katika majengo haya ya viwanja vya ndege kwa kuanzia TBI na hapa TBII,”
alisema Prof. Mbarawa.
Hatahivyo, aliyapongeza mashirika
na ofisi ambazo zimekuwa zikilipa kwa wakati fedha za pango, ambapo
uaminifu huo utawasaidia kupata nafasi katika jengo jipya la la tatu la
abiria, ambalo litakuwa linauwezo wa kuhudumia abiria milioni sita (6)
kwa mwaka.
Pia amewataka wale wasiowaaminifu
wachague kulipa madeni ya pango au wanaodaiwa na serikali au kuondoka,
ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengine ambao wanania ya dhati ya
kufanya biashara na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
wasimamizi wakuu wa viwanja vya serikali.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw.
Richard Mayongela alisema tayari zabuni mbalimbali zimeshatangazwa na
kuwataka wadau waliowaaminifu kujitokeza kuwania na kupata nafasi ya
kufanya shughuli zao kwenye eneo la JNIA.
“Tumeshatangaza zabuni hizo na
kama mhe. Waziri alivyosema zitakuwa za uwazi zikishirikisha wataalamu
na tunauhakika watapatikana watu wenye mapenzi mema ya kufanya biashara
na serikali” alisema Bw. Mayongela.
Katika hatua nyingine, Prof.
Mbarawa alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) na
kuridhishwa na kasi ya ujenzi, ambapo amewapongeza TAA, Tanroads na
Kampuni ya ujenzi ya Kimataifa ya Uholanzi (BAM).
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw.
Mayongela, alisema kukamilika kwa jengo hilo kutatoa fursa nyingi za
biashara zikiwemo uwekezaji katika hoteli, kumbi za mikutano, ofisi,
migahawa, maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali, huduma za kifedha (benki)
na karakana za ndege.
No comments:
Post a Comment