Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman
Jafo amesema kati ya wanafunzi 662,035 waliofaulu mtihani wa kumaliza
elimu ya msingi wanafunzi 650,862 sawa na asilimia 98.31
wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza katika awamu ya
kwanza mwaka 2018.
Akitangaza
matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka
2018 Tanzania Bara kwenye kikao na waandishi wa habari leo katika ofisi
za Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Jafo amesema kuwa
idadi wa wanafunzi mwaka huu imeongezeka kwa wanafunzi 124,209 ambapo
ni sawa na asilimia 23.58 ikilinganishwa na wanafunzi 526,653
waliochaguliwa awamu ya kwanza kuingia kidato cha kwanza mwaka 2016.
Amesema
kuwa wanafunzi 1912 wenye uhitaji maalum (pupils with special needs)
waliofaulu mitihani ya darasa la saba wamechaguliwa kujiunga na
masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2018 kwenye shule za sekondari za
Serikali.
Mhe.
Jafo amefafanua kuwa wanafunzi 11,173 sawa na asilimia 1.69 ya
waliofaulu hawakupata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha
kwanza katika awamu ya kwanza ya uchaguzi kutokana na uhaba wa
miundombinu ya elimu hususani vyumba vya madarasa kwenye baadhi ya
Halmashauri ya Mikoa ya Lindi (170), Mbeya (3,092), Rukwa (4,091),
Manyara (1,268), Katavi (976) na Simiyu (1,576).
Amesema
kuwa Halmashauri ambazo zimeshindwa kuwapangia wanafunzi wote
waliofaulu nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza ni Halmashauri za
Lindi wanafunzi (80) Mbeya (207),Halmashauri ya Jiji la Mbeya (
1,227), Mbarali (1,578), Kalambo (166), Nkasi (1,318), Halmashauri ya
Wilaya ya Sumbawanga (1,054), Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga
(1,553), Babati (581). Hanang (687), Mpanda (262), Nsimbo (714),
Halmashauri ya Mji wa Bariadi (369) na Halmashauri ya Wilaya ya Busega
(1,207).
Mhe.
Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa ambayo haijakamilisha ujenzi wa
miundombinu hasa ya vyumba vya madarasa kuhakikisha wanakamilisha hadi
kufikia mwezi februari, 2018 ili wanafunzi watakaochaguliwa kwenye awamu
ya pili wapate nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018.
“Lengo
la Serikali ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa
darasa la saba wanapata nafasi ya kujiunga na masomo ya kidato cha
kwanza nimeshatoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa
wanafunzi wote wanapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa
mwaka 2018” Amesema Jafo
Mhe.
Jafo amesisitiza kuwa walezi na wanafunzi ambao watakosa nafasi
katika awamu ya kwanza ya uchaguzi kuwa wavumilivu wakati mikoa
inajiandaa kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wote kuanza na masomo ya
kidato cha kwanza.
Amewaagiza
waalimu na watendaji wa elimu katika ngazi zote nchini kuongeza
bidii katika usimamiaji na ufuatiliaji wa utoaji wa elimu nchini na
kushirikiana na wadau wa elimu kukamilisha majengo na kuandaa
mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza 2018 bila vikwanzao vikiwemo michango na ada ili
kutekeleza sera ya utoaji wa elimu msingi bila malipo.
Aidha
amewaomba Wazazi, Walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Wilaya,
Halmashauri na shule, kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa
wanaandikishwa , wanahudhuria na kubaki shuleni hadi watakapohitimu
elimu ya Sekondari.
No comments:
Post a Comment