Mradi wa majaribio wa miezi 15 wa watoto waliokosa shule, kujifunza wenyewe kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayotumia tableti umezinduliwa mkoani Tanga.
Mradi huo uliozinduliwa katika kijiji cha Zenith ya Kati, wilayani Muheza ni sehemu ya mradi mkubwa wa miaka mitano wa majaribio duniani chini ya Global Learning Xprize wenye lengo la kutatua matatizo ya kujifunza.
Mradi huo hapa nchini unaendeshwa kwa pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na XPrize ambao wametoa tableti husika.
Aidha kuwezekana kuwapo kwa mradi huo kumetokana pia na makubaliano kati ya serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake ya elimu na TAMISEMI na mashirika.
Katika utoaji elimu huo watoto wanaohusika ni wa miaka kuanzia 9 hadi 11 na watajifunza kwa kutumia program tano zilizowekwa katika tableti zitakazomuwezesha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mradi huo wa Tanga ambao utagusa watoto 2,400 kutoka katika vijiji 167 vya wilaya za Handeni, Korogwe, Lushoto, Muheza, Mkinga na Pangani unatoa changamoto kwa timu ya wabunifu kuwezesha watoto walio na fursa ndogo ya kuingia katika elimu darasani kujifunza stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa kutumia tableti wakijifunza wenyewe. Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo katika kijiji cha Zenith, Muheza Mkoani Tanga, Mwakilishi wa Unesco ambaye pia anasimamia mradi huo Faith Shayo alisema kwamba mradi huo unaendana na majukumu ya Unesco ya kuhamasisha elimu jumuishi katika kuhakikisha kwamba watoto wote wa Tanzania wakiwemo wa jamii za pembezoni zilizo nyonge zinapata fursa.
Alisema UNESCO inatekeleza majukumu yake kwa kuisaidia serikali ya Tanzania kuwezesha kutoa elimu bora kwa wananchi wake wote na hata wale ambao hawana uwezo wa kupata elimu kutokana na mazingira yao au maeneo yao.
No comments:
Post a Comment