Mohamed Salah wa Misri amechaguliwa kuwa mshindi wa Tuzo ya BBC kwa Mwanakandanda Bora wa Afrika Mwaka 2017.
Nyota huyu wa Liverpool alipata
kura nyingi zaidi ya Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon, Naby Keïta wa
Guinea, Sadio Mané wa Senegal na mchezaji wa Nigeria Victor Moses.
“Nimefurahi sana kupata tuzo hii,” mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliiambia BBC Sport.
“Huwa ni hisia ya kipekee
unaposhinda kitu. Unahisi ulikuwa na mwaka mzuri sana. Kwa hivyo nina
furaha sana. Ningependa kushinda tena mwaka ujao!”
Salah, aliyefunga mabao mengi zaidi ligi kuu England, akiwa na mabao 13, amekuwa na mwaka wenye mafanikio.
Mapema 2017 alikuwa nyota wa Misri walipochukua nafasi ya pili katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Baadaye mwakani, mshambuliaji huyu
aliye na kasi alichangia katika magoli yote yaliyowasaidia Mafirauni
kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu
1990 – aliwasaidia wenzake kufunga mabao mawili, naye akafunga mabao
matano, moja ikiwa penalti kati yao na Congo iliyowawezesha kufuzu kwa
fainali hizo za Urusi.
“Ninataka kuwa mwanakandanda bora
zaidi wa Misri kwa hivyo mimi hutia bidii,” anasema kijana huyu ambaye
amekuwa raia wa tatu wa Misri kupata tuzo hii tangu 2008.
“Mimi hufuata njia yangu na ninataka watu wote Misri kufuata njia yangu”
Mchezo wake kwenye klabu yake umekuwa mzuri sana, sawa na ule wa nchi yake.
Nchini Italia, alifunga mabao 15
na kusaidia ufungaji wa mengine 11 na kuisaidia Roma kumaliza katika
nafasi ya pili kwenye Serie A, nafasi yao bora zaidi kwenye ligi katika
miaka saba, kabla ya kujiunga na Liverpool na kufunga bao mara 13 katika
mechi zao 16 za kwanza kwenye ligi.
“Ningependa kuwashukuru wenzangu
wa timu ya Liverpool na pia nilikuwa na msimu mzuri na Roma, kwa hivyo
lazima niwashukuru wenzangu huko na wale pia wa timu ya taifa,” alisema
Salah.
“Tangu nije hapa, nilitaka kujia
bidii sana na kuonyesha kila mtu uchezaji wangu. Nilitaka kurudi Ligi ya
Premia tangu nilipoondoka, kwa hivyo nina furaha sana.”
Salah amerejea Ligi ya Premia kwa
kishindi msimu huu, tofauti sana na alipokuwa kwenye ligi hiyo mara ya
kwanza akiwa na Chelsea kati ya 2014-15.
“Anastahiki,” anasema meneja wa
Liverpool Jurgen Klopp, aliyemkabidhi mchezaji huyo tuzo yenyewe katika
uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa Melwood.
“Kwa kweli mimi ni mtu mwenye
bahati sana. Nilikuwa na fursa ya kufanya kazi na wachezaji wachache wa
kipekee, wazuri, na nina furaha kwamba sasa nina Mo.
“Jambo zuri ni kwamba yeye bado
mdogo wa umri, anaweza kuimarika sana, ana uwezo mwingi ambao bado
tunaweza kuufanyia kazi, na hivyo ndivyo inafaa kuwa. Ni furaha sana
kwangu, kusema kweli, kufanya kazi naye.”
Salah sasa ameongeza jina lake
kwenye orodha ya wachezaji hodari kutoka Afrika, kama vile Abedi Pele,
George Weah, Jay-Jay Okocha na Didier Drogba, ambao wamewahi kushinda
Tuzo ya BBC kwa Mwanakandanda Bora wa Afrika wa mwaka.
“Nina furaha isiyo na kifani kuwa
kama wao katika kushinda tuzo hii,” amesema raia huyo wa Misri, ambaye
amewafuata raia wenzake Mohamed Barakat (2005) na Aboutreika (2008)
katika kushinda taji hilo.
No comments:
Post a Comment