Barua na video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza mbunge
wa Siha (Chadema) mkoani Kilimanjaro, Dk Godwin Mollel amejiuzulu ubunge
imezua mjadala.
Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema leo Alhamisi Desemba
14,2017 amesema naye ameona video na barua kwenye mitandao ya kijamii
lakini hawana uthibitisho wowote.
"Mheshimiwa Mollel hakuwahi kuonyesha dalili yoyote kuwa yuko kwenye
hilo wimbi na mimi nimeona hiyo barua na video kwenye mitandao. Bado
kwangu nachukulia kama uvumi mpaka tutakapothibitisha," amesema.
Lema amesema kwa utaratibu alipaswa kumuandikia barua Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe au viongozi wa Chadema.
Amesema akiwa katibu wa mkoa wa chama hicho hajapokea barua yoyote kutoka kwa Dk Mollel.
"Ukiangalia hata barua inayosambaa haijasainiwa na video inaonyesha ni
mtu tu kajirekodi akarusha. Katika mazingira hayo hatuwezi kukurupuka
kuzungumzia hilo jambo," amesema.
Taarifa inayosambaa kwenye mitandao ambayo haina saini inaonyesha
kuandikwa na Dk Mollel akieleza ameamua kujivua uanachama wa Chadema
kuanzia leo Alhamisi Desemba 14,2017.
Pia, ametangaza kujiuzulu nafasi ya ubunge na kwamba huo ni uamuzi wake
alioufanya akiwa na akili timamu na hajashinikizwa na mtu yeyote.
No comments:
Post a Comment