Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na ustawi wa wanyama nchini Tanzania—ASPA—limekutana na waandishi wa habari jijini Arusha kujadili mbinu bora za kukabiliana na tatizo la upotevu wa punda katika maeneo ya mipakani, hususan mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Shirika hilo limeeleza kuwa punda wameendelea kupotea kwa kasi, jambo linalodaiwa kusababishwa na biashara haramu ya mifugo na ukosefu wa udhibiti wa mipaka.
Katika mkutano huo, ASPA imeeleza kuwa punda ni miongoni mwa wanyama muhimu wanaotegemewa na jamii nyingi kwa shughuli za usafirishaji na uzalishaji, hivyo upotevu wao una athari kubwa za kiuchumi na kijamii.
Gladness Msemo, Afisa Elimu wa ASPA, amesema kuwa shirika hilo limekuwa likifanya utafiti katika maeneo mbalimbali ya mipakani na kubaini kuwa idadi ya punda wanaopotea imeongezeka kwa kiwango kinachotia wasiwasi.
"Tumeona ongezeko la matukio ya punda kupotea, hasa katika vijiji vilivyo jirani na mpaka wa Kenya. Hii ina madhara makubwa kwa wananchi wanaowategemea punda kwa shughuli zao za kila siku. Tunatoa wito kwa jamii kutoa taarifa mapema na kushirikiana katika kuwalinda wanyama hawa.”Gladness Msemo, Afisa Elimu ASPA.
Kwa upande wake, Robert Mbwambo, Afisa Ustawi wa Jamii wa ASPA, amesema shirika hilo limeandaa mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kukomesha tatizo hilo.
Amesema hatua zinazopendekezwa zinajumuisha kuimarisha ufuatiliaji wa mifugo, kushirikiana na mamlaka za mipakani, na kutoa elimu kwa jamii.
"Tunataka kuona mfumo madhubuti wa ufuatiliaji wa punda mipakani, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara. Punda hawa ni sehemu ya uchumi wa wananchi, hivyo jukumu la kuwalinda linapaswa kushirikisha kila mdau.”Robert Mbwambo, Afisa Ustawi wa Jamii ASPA.
Mwandishi wa habari Pendo Mkonyi amesifu hatua ya ASPA na kusisitiza jukumu la vyombo vya habari katika kuibua changamoto zinazohusiana na ustawi wa wanyama.
"Vyombo vya habari vinapaswa kuwa mstari wa mbele kuhabarisha jamii na kufuatilia kwa ukaribu matatizo kama haya. Upotevu wa punda si suala la kifamilia tu, ni suala la kijamii linalohitaji ushirikiano wa wadau wote.” Pendo Mkonyi, Mwandishi wa Habari.
ASPA imeahidi kuendelea kufanya tafiti, kutoa elimu na kushirikiana na serikali pamoja na jamii katika kukabiliana na tatizo la upotevu wa punda, ili kuhakikisha wanyama hao wanaendelea kulindwa na kutumika kama rasilimali muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment