Serikali imesema wanafunzi wa vyuo vikuu wanaongoza kutukana na kutumia lugha zisizo na maadili kwenye mitandao ya kijamii.
Angalizo hilo limetolewa na naibu waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha jana Jumamosi Machi
24, 2018 katika hafla fupi ya uzinduzi wa Unilife Compus iliyopo Mkoa wa
Kilimanjaro uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Mwenge na kuvikutanisha
vyuo vikuu vyote vya mkoa huo.
Amesema yapo mambo matatu ambayo
yanachangia wanafunzi kutofanya vizuri, yakiwamo matumizi mabaya ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), anasa na starehe
zilizopitiliza na kujiingiza kwenye siasa ambazo zinawanyima fursa ya
kusoma vizuri.
“Serikali imebaini mambo yanayochangia
kufifisha na kudidimiza jitihada za elimu tunayoitoa kuonekana bure.
Kuna vitu ambavyo siyo vizuri vinaendelea katika vyuo vyetu, ndizo
changamoto tunatakiwa kukabiliana nazo. Chuoni unaweza kutengeneza au
kuharibu maisha yako,” amesema.
Naye mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna
Mghwira amesema wanafunzi wengi hawataki kujifunza kwa kutumia muda
vizuri kwa kusoma vitabu.
"Tunabaki kuwa waigaji wa dhana za
wenzetu wa magharibi, hatutaki kujifunza vitu vipya bali vilevile vya
wenzetu vinatumika hadi leo. Wasomi wa Tanzania tunajishusha kwa sababu
ya kushindwa kuleta mawazo mapya kwenye sekta ya elimu na afya," amesema
Mghwira.
No comments:
Post a Comment