Kila mtu huwa na malengo, kila mwenye malengo hutamani
yafanikiwe. Hatahivyo watu wengi hufeli kutimiza malengo haya. Takwimu
zinaonesha kati ya watu takribani Bilioni 7.7 waliopo duniani ni
asilimia 5 tu kati yao ambao ni matajiri ambao utajiri wao huweza
kurithiwa na vizazi vyao vinavyowafuata.
Asilimia 15 kati yao ni wale wa uchumi wa kati, ambao maisha yao ni
ya kawaida, wanaweza kupata mahitaji yote muhimu ya maisha huku asilimia
80 ya watu wote duniani ni maskini yaani wanategemea kufanya kazi na
kupata fedha zinazoweza kuwakimu kwa siku au wanategemea msaada kutoka
kwa serikali za nchi zao.
Kutokana na hili wataalamu wa uchumi wameeleza kuwa zipo tabia ambazo
watu huziona za kawaida lakini tabia hizi husababisha umasikini. Ayo TV na millardayo.com inakuletea orodha ya tabia hizo kama ifuatavyo.
1. Kutumia muda mwingi kuangalia TV, sinema au tamthiliya
Dalili moja ya mtu kuwa masikini siku za mbeleni inatajwa kuwa
utaratibu wa kutumia muda mwingi kuangalia TV badala ya kufanya shughuli
za kuingiza kipato au hata shughuli za ziada zenye kuongeza manufaa
fulani hata kama sio pesa moja kwa moja.
Masaa mengi unayotumia kuangalia TV unaweza kuyatumia kufanya
shughuli za kibunifu, na kuutengenezea thamani muda wako. kuangalia TV
sio jambo baya lakini kutumia masaa mengi kuangalia TV, sinema au
tamthiliya ni hasara.
2. Kununua chakula (Fast food)
Hii ni tabia nyingine ambayo inatajwa ambayo kama hairekebishwi
hupelekea umaskini. Kama haukumbuki ni lini ulipika mwenyewe nyumbani
kwako kwasababu unanunua chakula wakati wote basi hiyo ni dalili mbaya.
Kwanza chakula cha fast food, kama pizza, burger, chipsi na
vinginevyo huwa na mafuta mengi na husababisha magonjwa kama uzito
uliopitiliza, magonjwa ya moyo n.k.
Haya yote hupunguza ufanisi wa mtu kufanya kazi vizuri ili afanikiwe
au afikie malengo yake. Madhara haya huathiri maeneo yote maisha,
kiuchumi, kiakili, kijamii na hata kimahusiano.
Tofauti na hilo, kununua vyakula hivi husababisha matumizi ya pesa
makubwa ambayo yanaweza kuepukika. Kwa mfano kama pizza moja ni sh elfo
20, mtu anaweza kutumia robo au theluthi ya pesa hiyo kununua chakula na
kupika mwenyewe mlo kamili yaani balanced diet.
3. Kuchelewa kuamka
Tabia hii kufanyika katika umri wa ujana inaelezwa kuwa ni dalili ya kuukaribisha umaskini katika siku za mbeleni.
Vijana ambao wanakuwa wazembe kufanya kazi kwa bidii kwenye kipindi
chao cha ujana, hufanya kazi zaidi na kwa tabu wakifika umri wa kuanzia
miaka 40 tena yawezekana bila malipo makubwa, na hii ni kwasababu
hawakutumia vizuri muda wao wa ujana kufanya kazi na kuwekeza kwa ajili
ya miaka ya mbeleni.
Inaelezwa kuwa watu matajiri, kama Bill Gates, Elon Musk, Mark
Zuckerberg na wengine, huamka mapema na kuanza kufanya kazi zao kwa
bidii kila siku, sasa kama matajiri ambao utajiri wao ni endelevu,
wanaona umuhimu wa kuamka mapema na kufanya kazi, vipi kuhusu kijana
anayeanza kutafuta maisha?
4. Kulaumu wengine kwa matatizo unayopitia
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa moja ya tabia zinazoweza kumfanya
mtu awe maskini ni pamoja na kulaumu watu wengine kutokana na
kutofanikiwa kwako.
Kuna msemo unaosema “Maisha ni jinsi unavyoamua kuyaona” hivyo kila
jambo linaweza kuwa ni la manufaa kwako aidha liwe zuri au baya,
kinafanya utofauti kati ya hayo mawili ni jinsi utakavyoamua
kulichukulia.
Jambo baya likitokea, masikini huwa wahanga wa jambo hilo lakini
matajiri hulitafakari, na kuangalia sababu halisi ya jambo hilo kutokea
kisha kuhakikisha halitokei tena au likitokea haliwaathiri au hata
kuhakikisha wanatumia fursa yoyote inayopatikana katika janga hilo ili
kunufaika nalo.
5. Kutoweka akiba
Akiba ni jambo la msingi sana katika mapato yoyote yanayopatikana.
Akiba ya pesa husaidia pindi likitokea tatizo, inaweza kuwa ugonjwa,
safari ya dharura na kadhalika. Kama huna akiba likitokea tatizo
itakubidi uuze mali yako yoyote au uchukue mkopo ili kutatua tatizo
hilo.
Tofauti na kutokea kwa matatizo, kama umeweka akiba na ikatokea fursa
ya wewe kutumia pesa ili kuingiza faida, utanufaika kuliko mtu asiye na
akiba, na huo ndio uzuri wa kutunza akiba ya pesa.
6. Kufanya manunuzi yasiyo kwenye mpangilio.
Hii ni pamoja na kununua vitu ambavyo havikuwa kwenye bajeti au
mpangilio. Kutokana na hili, wataalamu wanashauri kufanya manunuzi ukiwa
tayari umeandika orodha ya vitu unavyotaka kununua na sio kwenda sokoni
au dukani na kuangalia kilichopo ili ufanye manunuzi.
Pia ni kama kuchukua mkopo ili kununua vitu ambavyo havizalishi pesa,
kama kuchukua mkopo kununua furniture za ndani, au gari la kutembelea
na vinginevyo. hiyo ni hasara na hupelekea umasikini.
7. Kuzaa watoto wengi
Kama wewe ni kijana na una mpango wakuja kuwa na familia yenye watoto
wengi, hakikisha hali yako ya uchumi iko imara kabla haujaanza kuzaa
watoto hao.
Wataalamu wanaeleza kuwa kipato kikiwa kidogo na watoto wakiwa wengi
kwenye familia, kiwango cha umasikini kinaongezeka kwenye familia hiyo.
Inaelezwa kuwa matajiri wengi duniani, hawana watoto wengi japo kuwa
wanauwezo kifedha na wangeweza kuwahudumia, wanajua ni gharama kuwapa
watoto mahitaji yao yote ya msingi, tena kwa wakati.
Tajiri mkubwa duniani Bill gates ana watoto watatu, tajiri mwingine
Warren Baffet ana watoto 3, Mark Zuckerberg ana watoto wawili, na
kutokana na utajiri walionao, wanao uwezo wa kuwa na watoto zaidi ya
watano.
8. Kutopima afya mara kwa mara
Inawezekana ukaona sio suala la msingi kupima afya mara kwa mara
lakini hili ni suala la msingi kwa watu matajiri, kwani kuishi ukiwa na
uhakika wa afya ndio msingi wa kuishi maisha ya mafanikio.
Kupima afya mara kwa mara kunasaidia kujua mapema kama una ugonjwa
unaoanza mwilini mwako, hii ina faida kwani uwezekano wa kutibiwa na
kupona kabisa kwa ugonjwa huo ni mkubwa zaidi lakini pia gharama
utakazotumia kwa ajili ya matibabu zitakuwa nafuu kuliko ambazo
zingetumika wakati ugonjwa umekuwa mkubwa.
Ni kama ilivyo kwa ugonjwa wa saratani, kujua mapema ndio uhakika kwa
ugonjwa huo kutibiwa na kupona mapema tofauti na ukiwa umekomaa, au
hata ugonjwa wa kifua kikuu, au figo na magonjwa mengineyo.
9. Kutumia pesa kabla ya kuzipata
Kama una tabia ya kukopa pesa kipindi ambacho hauna pesa huku
ukitarajia kuzilipa pindi utakapopata pesa, hiyo ni dalili ya umaskini
kukunyemelea.
Kuepuka athari hii wataalamu wanashauri kufanya kazi kwanza na kupata
pesa kisha uendelee na kufanya matumizi ambayo unayahitaji.
10. Kuwa na marafiki wasio na malengo makubwa
Marafiki huweza kukusaidia kufikia malengo yako uliyojiwekea, lakini pia huweza kufanya usifikie malengo yako hayo.
Inashauriwa kuwa kama unataka kufanikiwa hakikisha unatumia muda
mwingi zaidi na marafiki ambao wana malengo makubwa ya maisha, wanawaza
mambo chanya na sio mambo hasi muda wote, ambao wanakukumbusha kufanya
vitu vya msingi.
Hii inaweza kuwa kutunza muda, kutokata tamaa kwenye malengo yako au
kuwa mbunifu zaidi, na hata kukukosoa kwa tabia ambazo zinarudisha
nyumba maendeleo yako.
No comments:
Post a Comment