Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo katika eneo la Nyahua wilayani Uyui Mkoani Tabora imesababisha kukatika kwa barabara kuu
ya Tabora kupitia Itigi hadi Dodoma na kusababisha magari ya abiria na
mizigo kwishindwa kuendelea na safari zake kwa kutumia barabara hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
katika eneo la tukio Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa
Tabora Mhandisi Damian Ndabalinze alisema mvua zilizonyesha katika
maeneo hayo zimesababisha kukatika kwa eneo hilo ambapo ndipo barabara
ya lami inaishia.
Aliwataka madereva wa magari ya aina
yoyote kudiriki kupita katika aina hilo kwa sababu wanaweza kuhatarisha
maisha yao na abiria na mizigo.
Ndabalinze alisema dereva yoyote
atakayekaidi na kuamua kupita katika eneo hilo kwa kulazimisha jambo
lolote litakalompata itakuwa ni yeye kajisababishia na asilelekeze
lawama kwa chombo chochote.
Alisema wakati taratibu nyingine
zikiendelea za kutaka kurejesha mawasiliano kwa kutumia barabara hiyo ni
vema magari yote ya kuja na kutoka Tabora yakapitia barabara ya Manyoni
, Singida , Nzega hadi Tabora.
“Natoa wito kwa magari ya kwenda
Kigoma na yale yanayoishia Tabora yapitie Nzega ili kuepusha usumbufu
kwa abiria na kwa madereva …kwani njia hii haipitiki tena,” alisema Meneja huyo.
Naye Afisa Mfawidhi wa SUMTRA Mkoa wa
Tabora Joseph Michael alisema kutokana na tatizo la kukatika kwa
barabara hiyo anatoa ruhusa kwa magari yote yaliyokuwa yakipitia
barabara ya Tabora kupitia Itigi hadi maeneo ya Dodoma na Dar es salaam
kuzungukia Nzega bila kibali kwa siku ya leo.
Alisema baada ya hapo wamiliki wanatakiwa kutafuta vibali ikiwa kama hali ya barabara hiyo itachelewa ili kuepuka usumbufu.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani Mkoani Tabora SP Emilian Kamuhanda alisema wamejipanga
kutoka matangazo katika Stendi kuu ya mabasi Tabora na kushirikiana na
Kikosi ya Usalama Barabara cha Mkoa wa Singida ili kuwaelekeza madereva
wote wapiti njia ya Nzega ili kuepuka usumbufu.
Kwa upande wa Mtendaji wa Kata ya
Kizenge Maganga Saulo alisema mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo
ilikuwa kubwa na kusababisha kukatika kwa eneo hilo , hatua iliyopelekea
magari kushindwa kupita.
Alisema ili kuhakikisha hakuna maafa yatakayotokea wanatumia Jeshi la Akiba kuwazuia madereva wanaotaka kujaribu kuvuka.
No comments:
Post a Comment