Pamoja na mkuu wa mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel kufika katika
eneo la tukio la machimbo ya dhahabu ya Nyakafuru wilayani Mbogwe na
kushuhudia wachimbaji wadogo wakilalamikia kikundi cha Isanjabadugu
kinavyowapora mawe yenye madini wachimbaji hao, hali ambayo RC huyo
ilimfanya kuagiza serikali wilayani humo pamoja na ofisi ya madini ya
mkoa kumaliza tatizo hilo lakini agizo hilo limeonesha kupuuzwa.
Katika ziara yake mhandisi Gabriel alionyesha kukerwa na tabia ya
unyanyasaji kwa wachimbaji wadogo wa machimbo hayo ingawa pamoja na
kumpata afisa madini afafanue lakini ufafanuzi wake haukumridhisha mkuu
huyo wa mkoa baada ya kuelezwa namna kikundi cha Isanjabadugu
kinavyowanyanganya mawe na kuwatoa kwenye machimbo wanayopata dhahabu
kwa kisingizio wao ndiyo wasimamizi walioteuliwa na serikali.
Juzi afisa madini mkazi wa mkoa wa Geita Ally Said alisema tayari
Jumatatu iliyopita alituma wataalamu wake kwenda kwenye machimbo hayo
kumaliza mgogoro huo lakini hadi kufikia jana kikundi hicho bado
kinaendelea kukusanya mawe asilimia 30 ya kila shimo hali ambayo
wachimbaji hao waliilalamikia mbele ya mkuu wa Mkoa huyo kwamba kikundi
hicho hakijawekeza rasilimali yoyote kwenye machimbo hayo lakini
kimekuwa kikichukua mawe mifuko 30 kwa kila shimo lenye mifuko 100.
Sabuni Jasaga ni mchimbaji anayemiliki shimo katika machimbo hayo ambaye
alisema kikundi hicho ni kama madalali wanaotumiwa na wakubwa kwa
kuwakusanyia pesa kwani wanaelewa kabisa Isanjabadugu hana eneo wala
hatumii gharama yoyote kwenye uchimbaji lakini ndiye anayechukua mawe
mengi kwa kisingizio cha usimamizi wa shughuli za uchimbaji.
“Ndugu mwandishi watu hawa wana pesa nyingi sana wamehonga kuanzia
wilaya hadi mkoa hivyo hata kama tungelalamikaje kikundi hicho
kinakusanya mawe kwa ajili ya wakubwa, hata wao wenyewe wanadai wako
kwenye mgongo wa viongozi wakubwa wa serikali haiwezekani waruhusiwe
kuvuna mawe yote hayo wakati anayefanya kazi ni mchimbaji ambaye ndiye
huteseka kupasua miamba lakini mawe yanapopatikana tayari isanjabadugu
hufika na kuchukua mgawo wao bila kazi yoyote huo ni unyonyaji”, alisema Jasaga.
Pamoja na hali hiyo mmiliki mwingine wa shamba katika eneo hilo Daud
Mabenga alisema walishaandika barua sehemu mbalimbali za serikali lakini
hakuna majibu hata wenyewe wenye mashamba kikundi hicho kikishachukua
mifuko 30 bure huwapa mifuko mitano tu huku 25 iliyobaki kudai ni mali
ya wakubwa ngazi ya Wilaya na Mkoa mbaya zaidi shimo hadi kulifikisha
kwenye mawe kazi hiyo hufanywa na zaidi ya watu 50 ambao huachiwa
asilimia 70.
Mabenga alisema katika asilimia hizo 70 huingizwa kodi mbalimbali wakati
mwingine kubaki na asilimia 40 ambayo hufanya waliopasuka mikono
kupasua miamba ya mawe kuambulia mfuko 1 watu wawili huku idadi kubwa
huchukuliwa na kikundi hicho ambao hawajui hata kushika nyundo kupasua
miamba na kwa siku wanauwezo wa kuvuna bila jasho mifuko zaidi ya 300.
Aliomba serikali iwaondoe kama alivyoagiza mkuu wa mkoa wa Geita
kumaliza tatizo hilo kwani kazi ya uchimbaji ni ngumu inapaswa kubaki
wachimbaji na mashimo yao na kodi za serikali mambo ya mtu kati
yaondolewe kwa kuwa kwa hapo Nyakafuru eneo hilo ni la mwekezaji sasa
hicho kikundi hakina maana yoyote kuwa dalali wa kukusanya mawe ya
wakubwa.
Alipotakiwa kuzungumzia hilo kamanda wa polisi mkoa wa Geita Mponjoli
Mwabulambo ambaye askari wake wa kituo cha Wilaya ya Mbogwe wamekuwa
wakituhumiwa kutumika kuwalinda na bunduki kikundi cha Isanjabadugu
wakati wa kukusanya mawe hayo, alisema suala hilo linashughulikiwa na
mkuu wa mkoa yeye hawezi kuliongelea kutokana na ngazi lilipo ni kubwa
ni kubwa hivyo alidai Mkuu huyu alishatoa maelekezo ya kulimaliza.
Nae mkuu wa wilaya ya Mbogwe Martha Mkupas alipotakiwa kuzungumzia namna
ya kikundi hicho kinachodaiwa kutumia pesa kuwahonga viongozi wote wa
wilaya na Mkoa ili kiendelee kukusanya mawe hayo, alidai madai hayo ni
ya uongo kwa kuwa wachimbaji wenyewe ndio waliochagua kisimamie shughuli
zote za uchimbaji ingawa alisema kama wataendelea kulalamika na kuleta
fujo atayafunga machimbo hayo kwa kuwa hayana mwenyewe eneo hilo ni la
mtafiti wa kampuni ya Mabango.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikundi hicho Joseph Warwa aligoma
kuzungumzia mgogoro huo licha ya mwandishi wa Blog hii kupiga kambi
mjini Ushirombo kwa siku tatu lakini Warwa alikuwa akiahidia kukutana
bila kuonekana hali ambayo mmoja wa viongozi wa kikundi hicho Evarist
Gervas alisema kikundi hicho sio kwamba kimetokea Geita bali ni muungano
wa wachimbaji kutoka Geita, Mbogwe na Bukombe ingawa hakuzungumzia
tuhuma za kujipatia bure mawe yanayochimbwa na wachimbaji kwa kusimamiwa
na serikali.
No comments:
Post a Comment