Unaweza
usiamini lakini huo ndiyo ukweli, ukisikia dunia ina maajabu basi haya
ni miongoni mwake.
Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Mora, Gujarat
nchini India, Jivunben Rabari mwenye umri wa miaka 70, siku chache
zilizopita ameushangaza ulimwengu baada ya kujifungua mtoto wake wa
kwanza katika umri huo na kuingia kwenye rekodi ya kuwa miongoni mwa
wanawake wachache waliokuja kupata watoto wakiwa tayari wameshazeeka.
Mwanamke
huyo alifunga ndoa na mumewe, Valjibhai Rabari takribani miaka 45
iliyopita lakini kwa kipindi chote hicho, licha ya kuhangaika sana,
hawakubahatika kupata mtoto katika ndoa yao.
Baada
ya kuhangaika sana, hatimaye walikutana na daktari Naresh Bhanushali
anayefanya kazi katika Kliniki ya Harsh IVF Centre mwanzo mwa mwaka huu
na kumueleza nia yao ya kutaka mtoto.
Akizungumza
na Gazeti la The National la nchini India, Daktari huyo amesema wazee
hao walipofika kwake na kumueleza shida yao, aliwakatalia na kuwaeleza
kwamba umri wao ulikuwa umeenda sana lakini wakasisitiza kwamba
wanachokitaka ni mtoto.
Daktari
huyo anazidi kueleza kwamba baada ya kuona msimamo wao bado upo
vilevile, aliamua kuwasaidia na baada ya kuumiza kichwa, aliamua
kujaribu njia ya kupandikiza ujauzito ambayo kitaalamu huitwa In Vitro
Fertilisation (IVF).
Katika
hali ambayo ilimshangaza hata daktari huyo, baada ya kukamilika kwa
hatua zote za kitaalamu zilizokuwa zinatakiwa, mwanamke huyo alipata
ujauzito ambao uliendelea kukua vizuri mpaka ulipotimiza miezi tisa na
hatimaye akajifungua kwa njia ya upasuaji.
Akieleza
tukio hilo kwa furaha, Jivunben alisema kwa miaka mingi walikuwa
wakihangaika kupata mtoto na hatimaye ndoto yao hiyo imetimia, jambo
ambalo wanaona ni kama muujiza kutoka kwa Mungu.
Mwanamke
huyo anaeleza kwamba enzi za ujana wao, madaktari walimwambia kwamba
hawezi kunasa ujauzito kutokana na matatizo aliyokuwa nayo katika mfumo
wake wa uzazi.
Septemba
2019, mwanamke mwingine nchini India, Mangayamma Yaramati, naye
aliushangaza ulimwengu baada ya kufanikiwa kujifungua salama watoto
pacha akiwa na umri wa miaka 74, naye akitumia teknolojia ya IVF kama
iliyotumika kwa wanandoa hao.
Japokuwa
inafahamika kwamba wanawake wengi hufikia ukomo wa hedhi wakiwa katika
umri wa kati ya miaka 40 hadi 50 na kufanya isiwezekane tena kwa wao
kupata ujauzito, maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwemo teknolojia
ya IVF, imewezesha wanawake wengi hata waliovuka katika umri wa ukomo wa
hedhi, kupata watoto.
No comments:
Post a Comment