
Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James amewataka vijana nchini kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Rais John Magufuli.
James
alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake aliyoitoa juzi mara baada ya
kutangazwa kuwa mshindi kuwataka wanachama kuifanyia kazi hotuba ya
mwenyekiti huyo wa CCM aliyoitoa wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa
UVCCM.
Katika
uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma, James aliibuka mshindi kwa
kupata kura 319 kati ya 583 zilizopigwa na kumwacha kwa mbali mpinzani
wake, Thobias Mwesiga aliyepata kura 127.
James
alitangazwa rasmi jana na msimamizi wa uchaguzi huo, William Lukuvi
kuwa mshindi wa nafasi hiyo iliyokuwa ikiwaniwa na wagombea saba. Wakati
akitangazwa, ulinzi ulikuwa umeimarishwa ndani ya ukumbi na mwenyekiti
huyo mpya alikuwa na walinzi.
“Kama
kuna kazi kubwa ya kufanya katika jumuiya yetu, basi ni kuhakikisha
tunapambana na rushwa. Tunakwenda kutekeleza agizo la Rais Magufuli mara
moja,” alisema James.
Ili
kuhakikisha hilo linafanyika kwa vitendo, James amewaagiza viongozi wa
umoja huo kuichapisha hotuba hiyo na nakala zake zisambazwe mikoani na
wilayani ili waanze kutekeleza maagizo ya kiongozi huyo ikiwamo
kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za jumuiya hiyo.
Katika
hotuba yake juzi, Rais Magufuli alisema UVCCM imekuwa dhaifu na
imegubikwa na vitendo vya rushwa ndiyo maana baada ya kuchaguliwa kwake
mwaka 2015, hakupelekewa orodha ya majina ya vijana wa umoja huo kwa
ajili ya kuteuliwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi serikalini hivyo
kutumia mbinu zake kuwatambua.
“Ninavyozungumza hapa mwenyekiti wenu (Sadifa Juma Khamis) yuko mahabusu kwa tuhuma za rushwa. Huo ndio umoja wa vijana?...”
Alisema
uelekeo ambao UVCCM ilikuwa ikienda si ule anaoufahamu wakati alipokuwa
mwanachama wake, hivyo inahitaji kufanyiwa marekebisho.
Kuhusu
mali za UVCCM, Rais Magufuli alisema zipo nyingi yakiwamo majengo
lakini zinatumika ovyo. Alitoa mfano jengo la umoja huo lililopo Dar es
Salaam ambalo haijulikani linakusanya mapato kiasi gani kwa mwaka.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema ni wakati wa bodi ya wadhamini ya UVCCM kuondoka kwa sababu haina msaada wowote kwa jumuiya hiyo.
Katika
uchaguzi huo, Thabia Mwita alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti kwa kura
286 dhidi ya mpinzani wake Rashid Mohamed Rashid ambaye alipata kura
282.
Wagombea
wengine waliochaguliwa ni mwakilishi wa vijana Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT), Dotto Nyirenda, mwakilishi wa vijana kwenda Jumuiya ya
Wazazi, Amir Mkalipa na wawakilishi watatu wa Tanzania Bara kwenda
Baraza Kuu la UVCCM ambao ni Rose Manumba, John Katarahiya na Secky
Kasuga.
Wengine
ni wawakilishi wawili wa Zanzibar kwenda Baraza Kuu la UVCCM ambao ni
Nasra Haji na Abdallah Rajabu. Pia wajumbe wawili kutoka Zanzibar
wanaokwenda Halmashauri Kuu ya Taifa, Abdallaghari Idrisa Juma na Maryam
Mohamed Khamis.
Vilevile
mkutano huo uliwachagua wajumbe wengine watatu kutoka Tanzania Bara
wanaokwenda Halmashauri Kuu ambao ni Sophia Kizigo, Mussa Mwakitinya na
Khadija Taya (Keisha).
No comments:
Post a Comment